Friday, 3 March 2017

SHAIRI :DAKTARI REJEA....

Siugui, ni unyonge mifupani
Siumwi, ni makuzi mwilini
Sifumbi, ni uzito machoni
Upo wapi nisisimke!

Nililala, n'kaota 'menijia
Nikakatula, n'kidhani meitikia,
Niligara, lipojua naotea
Upo wapi nisisimke!

Nilikuona, barasteni kipita,
Umebeba, mtungi ukanipita
Mwiba, moyoni n' kajuta
Upo wapi nisisimke!

Ukiniona, waogopa nashangaa
Ukinitazama, n'nabaki naduwaa
Waniogopa, akili zachuchumaa
Upo wapi nisisimke!

Nikiugua, naiona taswira
Waniuguza, uwele waupora
Wanibembeza, ugonjwa ukichakura
Upo wapi nisisimke!

Natamani, ngonjera tuziimbe
Pamojani, mwenyewe uambe
Kazini, meamua nirejee
Upo wapi nisisimke!

Tafadhali, utu sikutoke
Afadhali, maisha niokoe
Kulihali, maisha yazingatie
Upo wapi nisisimke!

Ketini, serikali muambizane
Mezani, mkataba mtingane
Sipitalini, mrejee sigombane
Upo wapi nisisimke!

Jubilee, si ugonjwa
NASA, si dawa
Maelewano, msije mkauuwa
Upo wapi nisisimke!
Daktari, rejea sipitalini,
Daktari, usitete ukaniuani
Daktari, utu rejeleeni
Upo wapi nisisimke!

Serikali, ilo moyoni
Serikali, jilegeze siniuweni
Ukubali, Daktari anijieni
Rejea Daktari wa moyoni...
  KUNTU!!!